PATANO LA VIONGOZI WAKUU WA MAKANISA WANACHAMA WA JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA KUHUSU NAFASI YAO KATIKA KUPAMBANA NA UGONJWA WA “COVID -19”

JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA

PATANO LA VIONGOZI WAKUU WA MAKANISA WANACHAMA WA JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA KUHUSU NAFASI YAO KATIKA KUPAMBANA NA UGONJWA WA “COVID -19”

Sisi viongozi wakuu wa Makanisa 13 wanachama wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania, katika kikao cha kutafakari nafasi yetu katika kupambana na tatizo la virusi vya korona, siku ya tarehe 29.04.2020, tumekubaliana kwa pamoja kufanya kama ifuatavyo:

KUIMARISHA HUDUMA MAKANISANI/WAJIBU WA WATUMISHI WA MUNGU

 1. Kutilia mkazo maombi kama  jambo la kwanza, ili Mungu atupe namna ya kukabiliana na tatizo la corona.  2Nyak7:14 ‘ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watatajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao’. Sisi Watumishi wa Kanisa ni muhimu kumlilia Mungu na kukubali kuwa tumekosea kwa mengi na kutubu kwa niaba ya kanisa na nchi; haijalishi nani amekosea. 
 2. Kuwatia moyo watu, sawasawa na neno la Mungu katika Isaya 40:1, ‘Watieni moyo watu wangu asema Bwana’, na kuwaelekeza katika tumaini.  Zab 46:1 ‘Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso’ Hofu inaleta mashaka,  hivyo ni muhimu tuone namna gani tunasaidia na kuwatia moyo  wakristo na watanzania kwa jumla katika kipindi  hiki cha tatizo la corona.  Vilevile tuwasaidie kiroho kwa kuwapa neno la Mungu.  Tutoe na huduma za kibinadamu pale inapobidi.
 3. Kuwaelekeza watukuchukua tahadhari zote na sisi wenyewe tuwe mfano.  Kila mmoja aone kwamba anao wajibu wa kujikinga na kuwakinga wengine.

 KUIMARISHA IBADA NA MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU

 1. Watu wapewe ruhusa ya kuhudhuria ibada kanisani au kubaki nyumbani na kufanya ibada huko, na kutuma sadaka zao kanisani kwa uaminifu. 
 2. Watoto wasije kanisani, familia ziweke utaratibu wa kuwafanyia ibada wakiwa nyumbani.  Wanaoenda kanisani wasiwadharau wasioenda, ila jambo la msingi ni kwamba wafanye ibada. 
 3. Tuhakikishe tunawalea wakristo wote kwa kuwafikishia ujumbe wa neno la Mungu kwa namna mbalimbali ikiwemo kutumia whatsapp, face book, youtube, na vipeperushi pale inapowezekana.  Hii ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuunda makundi  ya maombi kwa kutumia mitandao.  Pale ambapo teknolojia haipo basi familia zitumike kama nyumba za ibada na maombi.  Viongozi  wa Makanisa tusimame imara kuwasaidia watu wadumu na kuimarika katika imani yao.
 4. Ibada za kanisani ziwe za muda mfupi; kwa makanisa yenye watu wengi kuwe na awamu kadhaa za ibada zitakazotosheleza watu kukaa kwenye nafasi isiyo hatarishi yaani kiasi cha mita mbili baina ya mtu na mtu.  Watumishi wajipange kupokezana ibada kulingana na wingi wa watu.  Watu washauriwe kuwa wakitoka ibadani waende  kila mtu akakae nyumbani kwake.Tuhakikishe watu wanakuwa salama na masharti yanatekelezwa; kama kanisa hawawezi kutekeleza basi ni bora kufunga ibada.

KUJIKINGA NA KUWAKINGA WASHIRIKA DHIDI YA MAAMBUKIZI

 1. Kila Mchungaji ajitahidi kuchukua tahadhari zote. Hii nipamoja na kuvaa barakoa wakati wa kutoa huduma za kiroho, hata kama bado kuna baadhi ya wakristo wanaodhani kuwa unapovaa barakoa ni kama unamnyanyapaa.  Tuwape elimu kwa matendo, na kwamba sisi hatuwezi kuwakimbia, tutaendelea kuwapa huduma na  kukuza uelewa wao kuhusu corona huku na sisi pia tukijikinga.  Na watu wote wanaoenda kanisani kuabudu wavae barakoa hasa wakiwa kanisani. 
 2. Vifaa vyote vya kanisani vifanyiwe usafi kwa dawa ya kuvitakasa kabla ya ibada, ikiwemo magitaa, vipaza sauti, meza, viti, na vifaa vingine vitakavyotumika.  Waimbaji wasibadilishane  magitaa, na vipindi vya mazoezi visitishwe, ikiwemo na vipindi vingine; waimbe nyimbo ambazo wamezizoea na ambazo hazihitaji kuzifanyia mazoezi. 
 3. Kuombea wagonjwa: Neno la Mungu linaelekeza sio tu kuweka mikono juu ya wagonjwa, lakini hata kuwanyooshea mikono.  Kwa sababu ya corona tutumie kuwanyooshea mikono badala ya kuwagusa watu.
 4. Ibada za ndoa na sakramenti zingine zifanyike kwa uangalifu mkubwa ikiwemo kuwa na idadi ya  watu wachache,na kusiwepo sherehe.  Tuzingatie sana masharti yote ya kujikinga na kuwakinga watu wasipate maambukizi,  ibada isiwe mahali pa kusambaza corona.

KUJIELIMISHA NA KUTOA ELIMU:

 1. Tujifunze na tufundishe mafundisho sahihi na tuwasaidie watu kuepukana na  imani potofu kuhusu corona.  Tujazwe imani na maarifa, Wakolosai 1:9 ‘…mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni…’ .   Pasipo maarifa, watu huangamia, Hosea 4:6 ‘Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa’.  Kipindi hiki kinahitaji ufahamu na maarifa kutoka kwa Mungu.  Kuna mambo ya dua na maombi, lakini Mungu ametupa maarifa na busara pia, tunatakiwa kuitumia.  Tuzingatie  ushauri wa wataalam wa afya ili tupate ufahamu na maarifa yatakayotusaidia kufanya maamuzi sahihi.   Tusaidie kuwaelewesha watu waweze kuelewa.  Tuwe tayari kutoa majibu ambayo dunia imekosa.  Tutumie mtandao wa mawasiliano na kutoa masomo mafupi mafupi kwa washirika wetu.

WAJIBU WA CCT

 1. Pale itakapowezekana CCT isaidie upatikanaji wa vifaa kinga kama barakoa; kutengeneza na kusambaza vipeperushi; kuongeza matumizi ya redio, TV na mitandao ya kijamii kwa ajili ya kutoa elimu.
 2. Kushirikiana na kuhimiza Dayosisi na Makanisa kuvifikia vijiji kwa kuwapelekea vifaa kwa ajili ya huduma za usafi kwa ajili ya maandalizi ya ibada hasa maeneo ya  vijijini ambako shida kubwa ni pamoja na kukosa sabuni;  sambamba na kutoa elimu sahihi kuhusu janga la corona. 
 3. Kwa wazee na watu wasio na uwezo, makanisa yawe na akiba ya barakoa kwa ajili ya kuwawezesha kuabudu.
 4. Kushirikiana na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) ili kupata takwimu  na kuona uwezekano wa kuwa na mazungumzo na Serikali ili kusaidiana katika kupata ufumbuzi wa matatizo yanayozikabili hospitali za Makanisa.

KUSAIDIA NA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI

 1. Tupo tayari wakati wote kuisaidia serikali kwa njia mbalimbali ikiwemo kutambua na kutoa taarifa za wagonjwa na vifo vinavyohisiwa kuwa vimetokana na corona kwa kuzingatia mwongozo wa Wizara ya Afya.
 2. Kuwaelekeza  viongozi wa makanisa yetu, wachungaji, na wainjilisti wafahamu mwongozo wa kutolea taarifa, na kuwahimiza  kuwahudumia watu kwa uangalifu zaidi.
 3. Kuunda timu za wataalamu wa afya kwenye makanisa, ambazo zitasaidia na  kusimamia masuala mbalimbali ya kuhusu kupambana na corona kwa kushirikiana na wataalamu wa afya wa serikali kwenye maeneo yetu. 
 4. Kushiriki kuhimiza watu kujikinga dhidi ya maambukizi  kwa kutumia neno la Mungu na maarifa ya Mungu ikiwemo kuhimiza watu kukaa nyumbani, Isaya 26:20 ‘Njoni watu wangu, ingia wewe ndani ya vyumba vyako, ukafunge mlango nyuma yako ujifiche kitambo kidogo, mpaka ghadhabu hii itakapopita’.

USHAURI KWA SERIKALI

 1. Kwa watu wanaofariki kwa corona, ndugu zao wapewe majibu ya ugonjwa na wajulishwe kuhusu kifo kwa wakati ili kuondoa tatizo la baadaye la sonona.
 2. Serikali iendelee kutoa taarifa sahihi kwa wakati ili kusaidia watu kuujua ukweli wa hali ya maambukizi ili wafanye maamuzi sahihi kwa wakati sahihi.
 3. Ili kukabiliana na tatizo la unyanyapaa, tunatoa wito kwa Waziri wa Afya  pamoja na wataalam wake kuwa  wawe na programu maalumu kwenye runinga kuelezea hatari au madhara ya unyanyapaa ambao unaweza kusababisha vifo zaidi.  Kwa upande wetu viongozi wa makanisa tutaendelea kuelimisha watu kuhusu corona na madhara ya unyanyapaa.
 4. Watumishi, watendaji katika sekta ya afya wana hali ngumu na ya hatari kwa maana ya kuwa na upungufu wa vifaa tiba ikiwemo vifaa vya  kujikinga wenyewe wasipate maambukizi.  Tunatoa wito kwa watendaji wa Serikali,  natuwashauri kuwa kipaumbele namba moja cha fedha za michango zinazotolewa iwe kusaidia na kuwatunza watumishi wa sekta ya afya. 

Mwisho, tuko tayari kuendelea kushirikiana kupambana na tatizo la corona kwa kutumia hospitali na vituo vya afya vya Makanisa yetu.  Tunaomba Serikali iziiongezee nguvu hospitali na vituo vya afya vinavyomilikiwa na makanisa    ili ziweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa Corona.

PATANO hili limewekwa nasi viongozi wakuu wa Makanisa wanachama wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania, kwenye kikao cha kutafakariWajibu wetu katika kupambana na tatizo la corona, leo tarehe Ishirini na Tisa katika mwaka wa Bwana wetu Yesu Kristo Elfu Mbili na Ishirini.

 1. Askofu Dr. Alinikisa Cheyo               –           Mwenyekiti wa CCT
 2. Askofu Mkuu Dr. Frederick  Shoo   –           Makamu wa kwanza wa Mwenyekiti
 3. Rev. Canon Moses Matonya            –           Katibu Mkuu wa CCT
 4. Askofu  Musa Magwesela                            –           Kanisa la AICT
 5. Askofu Dismus Mofulu                                 –           Kanisa la Mungu
 6. Askofu Nelson Kisare                                    –           Menonite Church Tanzania
 7. Askofu  Philemon Tibanenason                   –           Kanisa la Pentekoste Tanzania
 8. Askofu Mkuu Dr. Maimbo W.Mndolwa –   Kanisa Anglikana Tanzania
 9. Askofu Conradi Nguvumali              –           Kanisa la Moravian Tanzania
 10. Askofu  John . Mchopa                                 –           Kanisa la Biblia
 11. Askofu  Josiah Samuel          -Baptist Convention of Tanzania, Kanda ya Pwani
 12. Rev. Julius Mwaitekele                                 –           Kanisa la uinjilisti Mbalizi
 13. Askofu Jacob Mameo                                   – KKKT Dayosisi ya Morogoro
 14. Askofu  Godfrey Sehaba                               – KAT Dayosisi ya Morogoro
 15.  Rev. John Kamoyo                            – CCT Idara ya Habari na Mawasiliano

Rev. Canon Moses Matonya

KATIBU MKUU WA CCT

Leave a Reply