Katika kuadhimisha maadhimisho ya siku ya nanenane (8 Agost 2025) Jumuiya ya kikristo Tanzania (CCT) imeendesha Kongamano kubwa la VICOBA wilayani Serengeti.

Vikundi 50 vya kuweka na kukopa toka vijiji vilivyoko ndani ya Wilaya ya Serengeti vimeweza kushiriki kongamano hilo lenye watu (wanavikundi) 1425 ambao wamehudhuria.
Ujumbe wa kongamano ni Vicoba huondoa umaskini na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia
Askofu Emmanuel Mwita Matuntera wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Jimbo la Serengeti
Amefungua kongamano hili kwa maombi ambapo katika ufunguzi wake amesoma kitabu cha
Zaburi 133 isemayo
“Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele.”
Nimesema maneno haya kwa sababu yanaendana na haya tunayofanya leo. Hapa tuna umoja Amani na mshikamano. Mungu awe nasi tunapoendelea ili tuweze kuzaa matunda, amesema.

Kongamano limeambatana na mafundisho mbalimbali yanayohusu uimarishwaji wa vikundi yaliyowasilishwa na wataalamu toka ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Justine Joseph ni Hakimu wa kituo cha Kenyana ameeleza kanuni na taratibu za kufuata wakati wakati wa usajili wa vikundi. Vikundi vitambuliwe kisheria, kupitia sharia ya vyama vya ushirika kwa kusimamia sharia ndogndogo za kikundi iitwayo katiba. Bila kuisajili katiba ni kazi bule maana mahakamani haiwezi kuwasaidia.
Hivyo mnapaswa kusajili muwe na wezo wa kutatua migogoro hata mahakamani. Hivyo mkisajili kisheria katiba basi kikoba kitakuwa na uwezo wa kumwadhibisha mtu ambaye hafuati kanuni zake mbele ya mahakama.
Jedilia Chiganga Afisa ustawi wa jamii na Maafisa wengine toka Dawati la jinsia wamewakumbusha juu ya ulinzi na usalama wa mtoto kwa wazazi wawapo katika shughuli za vikundi. Mtoto tunapaswa tumlinde kuendelea kizazi cha Taifa.
Kisheria mtoto anatambulika chini ya miaka 18, tuweke ulinzi kwa kuwapa haki zao za msingi , na sio kwenda kinyume kwa kuwafanyia vitendo visivyo sahihi kama ukeketaji. Mtoto akifanyiwa ukatili apelekwe kwenye nyumba salama zilizopo hapa Serengeti kwa uajili ya uangalizi. Mtoto ana haki ya kupata elimu bora na malezi bora. Tuachane na mila mbaya hasa za kukeketa, ambapo unamsababishia mtoto madhara kama kuvunja damu, kuambukiza magonjwa na vifo. Tulinde mila zetu za asili ila sio mila potofu kama ukeketaji.
Toa ripoti kwa viongozi ngazi ya kata au kijiji unapoona vitendo vya ukatili au kupiga simu bure kwa namba 116.
Paulina Edward toka Ustawi wa jamii amewasisitiza kuchangamkia fulsa ya usajili wa vikundi kwa kuwa sasa usajili ni bure. Hivyo hatuna sababu ya kuendesha vikundi bila kuvisajili. Kwenye mfumo wa serikali hatutambui vikundi ambavyo havisajiliwa. Hivyo fikeni ofisi zertu tuweze kuwasaidia, amesema. Amewasisitiza wanavikundi kuwa waaminifu katika kufanya marejesho, pia kuchukua mkopo na malengo maalumu ili kuondoa ugumu wa kufanya marejesho hasa pale mtu anakopa alafu pesa inatumika kinyume na malengo.
Sophia Mchomvu ni mratibu CCT wa Vikundi hivi ndani ya wilaya ya Serengeti, ameeleza wapi wametoka na wapi wanakwenda, akieleza mikakati ya vikundi kwa miaka mitatu ijayo.
Moja ni kuwa na kikundi cha pamoja cha kusaidizana wakati wa shida kupitia mfumo wa kisasa wa m-koba.
Mkakati mwingine ni kuwa na Benki ya vikundi vya Serengeti, benki ambayo itawasaidia hata kuajili vijana wao ambao sasa wanahitimu vyuo vikuu kwa hamasa na jitihada zao za kuhawamasisha wanavikundi kusomesha. Ameeleza nguvu ya vikundi akisema hadi sasa vikundi vina mtaji wa Tsh karibia bilioni mbili.
Lengo la tatu ni kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya ukatili kwa kipindi kifupi cha miaka ijayo.
Manufaa ya wanavikundi ni mengi katika kuwa kwenye vikundi hivi vya kuweka na kukopa
Leah Wambura toka kata ya Machocho ni mmoja wa wanufaika ambaye ameeleza namna alivyofaidi vicoba ikiwa ni pamoja na kujenga, kusomesha na kununua pikipiki mbili maarufu kama bodaboda kwa ajili ya kujiingizia kipato
. Wanufaika wengi wamepata nafasi ya kueleza mafanikio yao wengi ikiwa ni kuondoka katika nyumba za kupanga na kujenga nyumba zao wenyewe, kuanzisha biashara ndogondogo na kubwa na uwezo wa kujiamini katika kusimama mbele ya watu au kudai haki bila kuogopa.
Esther Muhagachi ni Mratibu CCT Idara ya wanawake ambaye ameeleza namna CCT inavyosimamia vikundi hivi na kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji vinaisha. Njia ambazo kwa sasa tumekuwa tukizitumia kufundishia ni kutoa madhara ya ukatili wa kijinsia kwa kutumia njia ya safari kwa wakati (time travel methods).
Tumeweza kutoa elimu kwa watoto shuleni kupitia klabu za watoto katika kupinga vitendo vya ukatili. Ameshukuru serikali kupitia idara mbalimbali hasa maendeleo ya jamii na ustawi ambao wamekuwa bega kwa bega katika kuimarisha shughuli za vikundi.

CCT tumefanikiwa kunusuru mabinti 800 juu ya ukeketaji. Tumefikia watu Zaidi ya efu 25 wamepokea elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Tumeelimisha watoto wa shule 16 za msingi na sekondari ambao ni 200 ambao nao wamefanikiwa kuelmisha watoto wenzao wapatao 9200 kwa njia ya nyimbo na ngonjera
Katika tamasha la sanday school tumeweza kufikia watoto 1400 juu ya ulinzi na usalama wa mtoto.
Tumeimarisha miradi ya pamoja kama mifungo, bustani, mradi wa samaki , maduka na vibanda vya kibiashara, miradi ya bodaboda na ujenzi kwa kauli ya JENGA TUPAUE PAMOJA.

Naye mgeni rasmi, Bi Happness John, Afisa tawala wilaya ya Serengeti akimwakilisha mkuu wa wilaya Mhe Angelina Marco Lubela ameishukuru CCT kunandaa kongamano hili.
CCT imejitoa sana katika kutoa elimu na hasa kupinga vitendo vya ukatili hasa ukeketaji. Mkoa wa mara umekuwa ukijihusisha sana na maswaa ya ukeketaji, kitendo kinachowakwamisha watoto wa kike kupata haki zao za msingi kama elimu. Amewaomba wana Serengeti kuwa na umoja katika kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya ukatikli wa kijinsia.
Wanawake wana haki ya kumili kama ardhi na mali. VICOBA vimetusaidia kupiga hatua ya wanawake kumiliki kupitia mafunzo yatolewayo CCT kwa kusaidizana na Serikali. VICOBA vinatusaidia kujiinua kiuchumi na hivyo wanawake kuondoa utegemezi kwa wanaume, amesema.
Amesisitiza wanaume kuendelea kuwapa nafasi wanawake kujiunga na vicoba katika kujiinua kiuchumi kupita mikopo. Amewasisitiza washiriki wa kongamano hili kuwa waaminifu katika kufanya marejesho wakati wanapochukua mikopo ili kuimarisha vicoba.